Saturday 31 March 2018

NGUVU YA KUOMBA MSAMAHA


Ingawa kuna wakati kuomba msamaha kunaonekana kama ni kitu kisichohitajika lakini ukweli ni kwamba kutokufanya hivyo kunaacha doa kubwa kuliko hata kosa ulilolifanya. Kuna nguvu katika kuomba msamaha ambayo ni kubwa kuliko maneno unayoyatamka.
Katika mafundisho yake katika mlima sermoni, Yesu alisema kuwa kama unaneno na ndugu yako na upo madhabahuni unataka kutoa sadaka, iache sadaka yako na uende kupatana naye kwanza kisha ndipo uje utoe sadaka yako.
Mathayo 5:23-24  Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako.
Hapa Yesu alimaaanisha kuwa kama umemkosea ndugu yako na hujamuomba msamaha haupaswi kufanya huduma yoyote mbele za Mungu. Haijalishi ni mtoto wako, mwenzi wako, mfanyakazi mwenzako, jirani n.k. Kuomba msamaha ni jambo gumu lakini lenye Baraka tele, kufanya hivi kutaimarisha uhusiano wako na uliyemkosea hata kama ni kwa bahati mbaya na pia kutaifanya nafsi yako kuwa huru na ya yule uliyemkosea pia.
Ni jambo baya sana kumhukumu mtu kwa jambo ambalo hajalitenda na kukataa kusikiliza upande wake wa habari na kuamini kile ulichokisikia au kuhisi. Pale unapogundua kuwa umemhukumu na kumsema mtu jambo ambalo hajafanya ni muhimu sana kumuomba msamaha kwa kutokumwamini, hii itamrejeshea heshima na upendo wake kwako na vilevile itarejeza uhusiano wenu. Inawezekana usione umuhimu wa kumuomba msamaha, lakini fahamu kuwa kutokuomba msamaha kutafanya uhusiano wenu kuwa mbaya na ni ngumu kwa mtu huyu kuachilia ulilomtendea.
Kuomba msamaha kunaondoa ile hasira aliyonayo mtu uliyemkosea na hata kama kosa ni kubwa kuomba kwako msamaha kutamfanya afikirie upya maanuzi yake na hasira yake itapungua kwa kiasi kikubwa. Ni ngumu sana kwa mtu aliyeombwa msamaha kuendelea kuwa na hasira na uchungu na Yule aliyemkosea tofauti na yule ambaye hajaombwa msamaha. Hata kama akikataa kutoa msamaha wake tatizo halitakuwa kwako tena bali kwake, moyo wako utakuwa safi na itabaki sasa yeye na moyo wake maana umeonyesha kujali kosha ulilolifanya na kulitubia.
Kumbuka, kuomba msamaha hakutakiwi kuwe ni njia ya kumlazimisha mtu uliyemkosea kukusamehe. Kama kuomba kwako msamaha kutakuwa kwa kulazimisha, kwa dharau au dhihaka au kusikomaanisha bali kwa kutimiza sheria tu kunaweza kusababisha maumivu zaidi kwa yule uliyemkosea na kuchochea hasira zaidi badala ya msamaha. Kuomba msamaha si maneno tu bali pia na vitendo vinavyofuatia na hata jinsi unavyoomba msamaha wenyewe. Maanisha kweli unachokisema na maneno yako, sauti na mwonekano mzima uonyeshe kweli umejutia kosa lako na unahitaji msamaha.
Pia usichelewe kuomba msamaha baada ya kugundua kuwa umefanya kosa. Watu wengine hawaombi msamaha hadi wasukumwe kwa maneno meengi au aone mtu amenuna na kuacha kuongea naye. Hauwezi kukaa kimya tu kama hakuna kitu kilichotokea na kutegemea kuwa jambo hilo litaisha lenyewe, unapaswa kuomba msamaha pale tu unapoona umekosea. Unapochukua muda mrefu kuomba msamaha maumivu kwa yule mtu yanazidi na hata pale unapoomba msamaha inakuwa vigumu kwake kukusamehe maana umeacha mambo yakazidi kukua ndani yake.
Ubarikiwe na Bwana Yesu unapochukua hatua na kuomba msamaha pale unapokosea. 

Kwa ushauri/maoni tunaweza kuwasiliana kwa e-mail:fkmwamoto@gmail.com au Whatsapp 0784190882.


Wednesday 21 February 2018

FAIDA ZA KUSAMEHE

1. Kwanza kabisa, tunasamehe kwa sababu kusamehe ni amri na ni agizo la Mungu. binadamu ni watu ambao hawapendi kukubali kosa ni watu waliozoea kujitetea na kukataa kosa pale anapokosa. Kama tukikataa kutii tunakaidi agizo la Mungu hivyo tunapaswa kusameheana kwani muasisi wa msamaha ni Mungu mwenyewe na kama Mungu angehesabu maovu yetu nani angesimama? Anza leo kusamehe, hakuna aliye mkamilifu.
2. Tunasamehe ili tuweze kusamehewa na pia ili maombi yetu yaweze kupokelewa na Mwenyezi Mungu. Unapaswa kusamehe kwa faida yako mwenyewe siyo kwa faida ya mkosaji na mwachie Mungu apambane na watesi wako wala usilipe kisasi wewe mwekee mtesi wako kaa la moto kichwani limchome. Kumwekea kaa la moto kichwani ni kama kumtesa kisakikolojia wewe unamsamehe yeye, amini basi nafsi yake inaendelea kumtafuna.
3. Unasamehe ili uwe na Amani ya moyoni mwako. Unaposamehe unakuwa unapata amani ya moyo. Mtu ambaye anavumilia uchungu ulioumbika ndani ya moyo na hataki kuachilia fundo hilo lazima litamtesa na atakosa amani ya moyo. Atahangaika na huku uchungu ulioumbika ndani ya moyo ukiendelea kumtafuta.
4. Unasamehe ili uwe na furaha moyoni mwako. Kwa kweli ukiangalia watu wanaokataa kusameheana huwa hawana furaha kabisa katika mioyo yao. Kama unaishi katika mahusiano yoyote na mara nyingi huwa watu si wakamilifu basi msamaha ndio kiunganishi chenu ambao utarudisha uhusiano uliopotea au uliovunjika na kuleta uhusiano wa awali yaani uhusiano mpya.

5. Tunasamhe ili tuwe na afya njema. Uponyaji wa kweli unaanzia moyoni. Kama mtu anasamehe kutoka moyoni basi huo ni msamaha wa kweli na ni msamaha unaongozwa na huruma ya Mungu ndani yake. Watu hawataki kusamehe ndio maana wengine afya zao ni dhaifu. Uchungu ulioumbika ndani ya moyo unaendelaa kumtafuna. Usizeeke kabla ya wakati kwa ajili ya kutosamhe.
6. Kutosamhe kunakufanya ujikinai wewe mwenyewe. Unajiona wewe ni mtu ambaye hustahili kuwepo hapa duniani. Utajiona wewe hauna maana hapa duniani utakua unakaa peke yako peke yako. Huna furaha, amani, upendo. Maisha yako yanakuwa yamejaa sumu na majeraha moyoni ugonjwa umekuwa mkubwa na wewe hutaki kuupatia dawa ya kuuponya na dawa yake ni msamaha tu.
7. Kutokusamhe kunaongeza maadui katika maisha yako. Kuna faida kubwa sana ya kusamehe. Jaribu kuangalia katika maisha yako Yule anayesamehe na asiyesamehe nani anakuwa anaongeza maadui? Utaongeza maadui na utavunja uhusiano na watu hivyo utakua unaishi maisha ya umimi. Maisha ya binadamu ni maisha yenye uhusiano kama husamehi basi unajitengenezea duniani yako mwenyewe.
8. Kutosamhe kunaleta mapasuko wa kifamilia. Katika hali ya kawaida jaribu kuangalia katika jamii yako ni familia ngapi zimesambaratika kwasababu ya kutosameheana ? ni nyingi sana kwanza familia nyingi zina migogoro ya aina mbalimbali inayosababishwa na watu kulipiana visasi na kutosameheana na kuishi maisha ya chuki kama ya paka na panya. Kusamehe ni faida kwa kila familia bora inayotaka amani na furaha, mipasuko katika familia itaendela kuwepo kama watu wasiposameheana.
9. Kutosamhe kunaleta unyonge wa moyo yaani huzuni. Ukiwaangalia watu wengine unawaonea huruma wanaishi maisha ya huzuni wakati falsafa ya maisha ni furaha hapa duniani. Tunatafuta kila siku ili tuweze kuwa na furaha. Inuka leo na nenda kazike hilo jeneza la huzuni na kuwa huru na maisha yako. Huoni ni utumwa kuwabeba watu moyoni? Hujaja duniani kuteseka na maisha ni mafupi sana samehe na endelea na maisha yako.
10. Kutosamhe kunawafanya watu kukimbia makazi na ofisi zao. Kwa mfano, watu waliokoseana na hawataki kusameheana huwa wanaishi maisha kama ya paka na panya. Akimuona mwenzake huyo anakuja anakimbia kama yuko nyumbani anakimbia, kama ni njia anabadilisha kabisa ili wasionane na kusalimiana. Unakuta watu wengine wanakimbia kabisa ofisi zao kwa sababu ya kutotaka kusameheana. Kwanini uendelea kuishi maisha haya? Anza kubadilika kama ulikuwa unakimbia makazi au ofisi ili usikutane na mtesi wako.

Maisha ya kutokusamehe yanahasara nyingi na faida ni nyingi zaidi kuliko hasara. Imani za watu zinakufa kwa ajili ya kutokusamehe, watu wanazeeka mapema kabla ya muda, watoto wa mitaani wanaongezeka kwa ajili ya kutokusamehe yaani; pale wazazi wanapotalakiana na kuwatelekeza watoto. Tuishi katika maisha ya kusameheana na siyo ya kulipizana visasi.


Kwa ushauri tuwasiliane kwa barua-pepe fkmwamoto@gmail.com au Whatsapp 0784190882

Wednesday 3 January 2018

MAHUSIANO KWA MWAKA 2018

Leo ni siku ya tatu(3) tangu tuanze mwaka 2018, ili kudumisha na kuboresha mahusiano yetu kwa mwaka huu mpya. Napenda kuwashauri kuishia kwa kanuni zifuatazo: -
©       Kuacha kuangalia madhaifu kwa mwenza wako, bali tuangalie mazuri ya mwenza wako.
©       Tumuombe Mungu atupe uwezo wa kusamehe, ili maombi yetu yaweze kupokelewa na Mungu wetu
©       Kuepuka kushirikisha watu wengi kwenye husiano wetu bali tumshirikishe Mungu msimamizi na muasisi wa uhusiano na ndoa.
©       Jitahidi kuwaelewa wenzetu badala ya kutaka wenzetu kutuelewa sisi.
©       Tuheshimu matumizi ya muda kwa maana ni raslimali muhimu sana katika maisha yetu.
©       Shirikiana na kila mtu unayekutana naye kwa maana kila mwanadamu ni muhimu kwako kama siyo kwa leo ni kwa siku za baadae.

Naomba kwa leo tuishie hapo.