Saturday, 31 March 2018

NGUVU YA KUOMBA MSAMAHA


Ingawa kuna wakati kuomba msamaha kunaonekana kama ni kitu kisichohitajika lakini ukweli ni kwamba kutokufanya hivyo kunaacha doa kubwa kuliko hata kosa ulilolifanya. Kuna nguvu katika kuomba msamaha ambayo ni kubwa kuliko maneno unayoyatamka.
Katika mafundisho yake katika mlima sermoni, Yesu alisema kuwa kama unaneno na ndugu yako na upo madhabahuni unataka kutoa sadaka, iache sadaka yako na uende kupatana naye kwanza kisha ndipo uje utoe sadaka yako.
Mathayo 5:23-24  Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako.
Hapa Yesu alimaaanisha kuwa kama umemkosea ndugu yako na hujamuomba msamaha haupaswi kufanya huduma yoyote mbele za Mungu. Haijalishi ni mtoto wako, mwenzi wako, mfanyakazi mwenzako, jirani n.k. Kuomba msamaha ni jambo gumu lakini lenye Baraka tele, kufanya hivi kutaimarisha uhusiano wako na uliyemkosea hata kama ni kwa bahati mbaya na pia kutaifanya nafsi yako kuwa huru na ya yule uliyemkosea pia.
Ni jambo baya sana kumhukumu mtu kwa jambo ambalo hajalitenda na kukataa kusikiliza upande wake wa habari na kuamini kile ulichokisikia au kuhisi. Pale unapogundua kuwa umemhukumu na kumsema mtu jambo ambalo hajafanya ni muhimu sana kumuomba msamaha kwa kutokumwamini, hii itamrejeshea heshima na upendo wake kwako na vilevile itarejeza uhusiano wenu. Inawezekana usione umuhimu wa kumuomba msamaha, lakini fahamu kuwa kutokuomba msamaha kutafanya uhusiano wenu kuwa mbaya na ni ngumu kwa mtu huyu kuachilia ulilomtendea.
Kuomba msamaha kunaondoa ile hasira aliyonayo mtu uliyemkosea na hata kama kosa ni kubwa kuomba kwako msamaha kutamfanya afikirie upya maanuzi yake na hasira yake itapungua kwa kiasi kikubwa. Ni ngumu sana kwa mtu aliyeombwa msamaha kuendelea kuwa na hasira na uchungu na Yule aliyemkosea tofauti na yule ambaye hajaombwa msamaha. Hata kama akikataa kutoa msamaha wake tatizo halitakuwa kwako tena bali kwake, moyo wako utakuwa safi na itabaki sasa yeye na moyo wake maana umeonyesha kujali kosha ulilolifanya na kulitubia.
Kumbuka, kuomba msamaha hakutakiwi kuwe ni njia ya kumlazimisha mtu uliyemkosea kukusamehe. Kama kuomba kwako msamaha kutakuwa kwa kulazimisha, kwa dharau au dhihaka au kusikomaanisha bali kwa kutimiza sheria tu kunaweza kusababisha maumivu zaidi kwa yule uliyemkosea na kuchochea hasira zaidi badala ya msamaha. Kuomba msamaha si maneno tu bali pia na vitendo vinavyofuatia na hata jinsi unavyoomba msamaha wenyewe. Maanisha kweli unachokisema na maneno yako, sauti na mwonekano mzima uonyeshe kweli umejutia kosa lako na unahitaji msamaha.
Pia usichelewe kuomba msamaha baada ya kugundua kuwa umefanya kosa. Watu wengine hawaombi msamaha hadi wasukumwe kwa maneno meengi au aone mtu amenuna na kuacha kuongea naye. Hauwezi kukaa kimya tu kama hakuna kitu kilichotokea na kutegemea kuwa jambo hilo litaisha lenyewe, unapaswa kuomba msamaha pale tu unapoona umekosea. Unapochukua muda mrefu kuomba msamaha maumivu kwa yule mtu yanazidi na hata pale unapoomba msamaha inakuwa vigumu kwake kukusamehe maana umeacha mambo yakazidi kukua ndani yake.
Ubarikiwe na Bwana Yesu unapochukua hatua na kuomba msamaha pale unapokosea. 

Kwa ushauri/maoni tunaweza kuwasiliana kwa e-mail:fkmwamoto@gmail.com au Whatsapp 0784190882.


Wednesday, 21 February 2018

FAIDA ZA KUSAMEHE

1. Kwanza kabisa, tunasamehe kwa sababu kusamehe ni amri na ni agizo la Mungu. binadamu ni watu ambao hawapendi kukubali kosa ni watu waliozoea kujitetea na kukataa kosa pale anapokosa. Kama tukikataa kutii tunakaidi agizo la Mungu hivyo tunapaswa kusameheana kwani muasisi wa msamaha ni Mungu mwenyewe na kama Mungu angehesabu maovu yetu nani angesimama? Anza leo kusamehe, hakuna aliye mkamilifu.
2. Tunasamehe ili tuweze kusamehewa na pia ili maombi yetu yaweze kupokelewa na Mwenyezi Mungu. Unapaswa kusamehe kwa faida yako mwenyewe siyo kwa faida ya mkosaji na mwachie Mungu apambane na watesi wako wala usilipe kisasi wewe mwekee mtesi wako kaa la moto kichwani limchome. Kumwekea kaa la moto kichwani ni kama kumtesa kisakikolojia wewe unamsamehe yeye, amini basi nafsi yake inaendelea kumtafuna.
3. Unasamehe ili uwe na Amani ya moyoni mwako. Unaposamehe unakuwa unapata amani ya moyo. Mtu ambaye anavumilia uchungu ulioumbika ndani ya moyo na hataki kuachilia fundo hilo lazima litamtesa na atakosa amani ya moyo. Atahangaika na huku uchungu ulioumbika ndani ya moyo ukiendelea kumtafuta.
4. Unasamehe ili uwe na furaha moyoni mwako. Kwa kweli ukiangalia watu wanaokataa kusameheana huwa hawana furaha kabisa katika mioyo yao. Kama unaishi katika mahusiano yoyote na mara nyingi huwa watu si wakamilifu basi msamaha ndio kiunganishi chenu ambao utarudisha uhusiano uliopotea au uliovunjika na kuleta uhusiano wa awali yaani uhusiano mpya.

5. Tunasamhe ili tuwe na afya njema. Uponyaji wa kweli unaanzia moyoni. Kama mtu anasamehe kutoka moyoni basi huo ni msamaha wa kweli na ni msamaha unaongozwa na huruma ya Mungu ndani yake. Watu hawataki kusamehe ndio maana wengine afya zao ni dhaifu. Uchungu ulioumbika ndani ya moyo unaendelaa kumtafuna. Usizeeke kabla ya wakati kwa ajili ya kutosamhe.
6. Kutosamhe kunakufanya ujikinai wewe mwenyewe. Unajiona wewe ni mtu ambaye hustahili kuwepo hapa duniani. Utajiona wewe hauna maana hapa duniani utakua unakaa peke yako peke yako. Huna furaha, amani, upendo. Maisha yako yanakuwa yamejaa sumu na majeraha moyoni ugonjwa umekuwa mkubwa na wewe hutaki kuupatia dawa ya kuuponya na dawa yake ni msamaha tu.
7. Kutokusamhe kunaongeza maadui katika maisha yako. Kuna faida kubwa sana ya kusamehe. Jaribu kuangalia katika maisha yako Yule anayesamehe na asiyesamehe nani anakuwa anaongeza maadui? Utaongeza maadui na utavunja uhusiano na watu hivyo utakua unaishi maisha ya umimi. Maisha ya binadamu ni maisha yenye uhusiano kama husamehi basi unajitengenezea duniani yako mwenyewe.
8. Kutosamhe kunaleta mapasuko wa kifamilia. Katika hali ya kawaida jaribu kuangalia katika jamii yako ni familia ngapi zimesambaratika kwasababu ya kutosameheana ? ni nyingi sana kwanza familia nyingi zina migogoro ya aina mbalimbali inayosababishwa na watu kulipiana visasi na kutosameheana na kuishi maisha ya chuki kama ya paka na panya. Kusamehe ni faida kwa kila familia bora inayotaka amani na furaha, mipasuko katika familia itaendela kuwepo kama watu wasiposameheana.
9. Kutosamhe kunaleta unyonge wa moyo yaani huzuni. Ukiwaangalia watu wengine unawaonea huruma wanaishi maisha ya huzuni wakati falsafa ya maisha ni furaha hapa duniani. Tunatafuta kila siku ili tuweze kuwa na furaha. Inuka leo na nenda kazike hilo jeneza la huzuni na kuwa huru na maisha yako. Huoni ni utumwa kuwabeba watu moyoni? Hujaja duniani kuteseka na maisha ni mafupi sana samehe na endelea na maisha yako.
10. Kutosamhe kunawafanya watu kukimbia makazi na ofisi zao. Kwa mfano, watu waliokoseana na hawataki kusameheana huwa wanaishi maisha kama ya paka na panya. Akimuona mwenzake huyo anakuja anakimbia kama yuko nyumbani anakimbia, kama ni njia anabadilisha kabisa ili wasionane na kusalimiana. Unakuta watu wengine wanakimbia kabisa ofisi zao kwa sababu ya kutotaka kusameheana. Kwanini uendelea kuishi maisha haya? Anza kubadilika kama ulikuwa unakimbia makazi au ofisi ili usikutane na mtesi wako.

Maisha ya kutokusamehe yanahasara nyingi na faida ni nyingi zaidi kuliko hasara. Imani za watu zinakufa kwa ajili ya kutokusamehe, watu wanazeeka mapema kabla ya muda, watoto wa mitaani wanaongezeka kwa ajili ya kutokusamehe yaani; pale wazazi wanapotalakiana na kuwatelekeza watoto. Tuishi katika maisha ya kusameheana na siyo ya kulipizana visasi.


Kwa ushauri tuwasiliane kwa barua-pepe fkmwamoto@gmail.com au Whatsapp 0784190882

Wednesday, 3 January 2018

MAHUSIANO KWA MWAKA 2018

Leo ni siku ya tatu(3) tangu tuanze mwaka 2018, ili kudumisha na kuboresha mahusiano yetu kwa mwaka huu mpya. Napenda kuwashauri kuishia kwa kanuni zifuatazo: -
©       Kuacha kuangalia madhaifu kwa mwenza wako, bali tuangalie mazuri ya mwenza wako.
©       Tumuombe Mungu atupe uwezo wa kusamehe, ili maombi yetu yaweze kupokelewa na Mungu wetu
©       Kuepuka kushirikisha watu wengi kwenye husiano wetu bali tumshirikishe Mungu msimamizi na muasisi wa uhusiano na ndoa.
©       Jitahidi kuwaelewa wenzetu badala ya kutaka wenzetu kutuelewa sisi.
©       Tuheshimu matumizi ya muda kwa maana ni raslimali muhimu sana katika maisha yetu.
©       Shirikiana na kila mtu unayekutana naye kwa maana kila mwanadamu ni muhimu kwako kama siyo kwa leo ni kwa siku za baadae.

Naomba kwa leo tuishie hapo.

Friday, 19 May 2017

MAZOEA SABA (7) MABAYA KWA WANANDOA

Napenda tena kuchukua nafasi hii adimu kumshukuru Mwenyezi Mungu muumba wa mbingu na nchi kwa kunipa nafasi ya kuwasilisha kwenu baadhi ya mazoea mabaya ustawi ndoa ambayo hufanywa na wanandoa wengi. Pia napenda kuwashukuru wale wote waliopata nafasi ya kusoma makala zangu kwa maoni na mawazo yenu mazuri, napenda kuchukua nafasi hii kuwaombeni mwaalike na wenzenu kusoma makala zangu ambazo huwa natoa kila wiki.
Leo nitaongelea makosa saba (7) ambayo mara nyinyi hufanywa na wanandoa na kusababisha kuibuka kwa migogoro katika mahusiano. Makosa hayo ni kama yafuatavyo: -
1.   Kususia tendo la ndoa bila sababu ya msingi; Tendo la ndoa ni mmojawapo wa nguzo muhimu ya ndoa zote. Kwa hiyo, inapotokea mmoja wa wanandoa kuamua kumnyima mwenzake tendo la ndoa bila sababu ya msingi ni tendo ambalo linaweza kusababisha kuvunjika kwa ndoa bila kujali ni ya kidini, kimila au kiserikali.
2.   Kumsema vibaya mwenzako wako kwa rafiki/ndugu; Ni makosa makubwa sana kwa mustakabali wa ndoa kwa mmoja wa wanandoa kumsema vibaya mwenzake kwa rafiki zake au ndugu zake badala ya kumuelimisha ili kuondoa  kasoro unazoziona kwake.
3.   Kutotimiza yale unayosema; Ni kosa kubwa sana kwa mwanandoa kutotimiza/kutenda yale anayoahidi kwa mkewe/mmewe bila sababu ya msingi. Katika mahusiano hutokea misukosuko ya hapa na pale na nyingi hutokea mmoja wa wanandoa kuomba msamaha na kukiri kutorudia vitendo fulani ambavyo ni kero kwa mwenzako kwa mfano; kulala nje, kuchelewa kurudi nyumbani bila taarifa yo yote, nakadhalika.
4.   Kutokukubali makosa; Ni busara kwa mstakabali mzuri wa ndoa kukubali makosa inapotokea kuwa mmoja wa wanandoa kafanya makosa. Imekuwa ni vigumu sana kwa wanandoa hasa wanaume kukubali makosa inapotokea wamefanya makosa na badala yake huonyesha kukiri kwa vitendo yaani; kufuata mapendekezo ya wake zao na siyo kukubali kwamba maamuzi yao ya awali yalikuwa na makosa. Si dhambi kukiri kufanya maamuzi kimakosa inapotokea kwa mustakabali mwema wa mahusiano.
5.   Kuwa na hasira zisizo na mpangilio; Ni makosa makubwa kuwa na hasira zisizo na mpangilio kwa mwenzako au kuhamisha hasira kutoka ofisini au kwenye shughuli yo yote unayoifanya na kuzipeleka nyumbani.
Nyumbani ni mahali ambapo inakiwa iwe ni pakupatia faraja na pumziko stahili.
6.   Kutojishughulisha na kumuelewa mwenzako; Ni jambo jema kwa mustakabali mzuri mahusiano kufanya jitihadi kumuelewa mwenzako anakuweje katika hali ya furaha au huzuni. Hili ni muhimu sana katika mahusiano hata katika urafiki wa kawaida. Hii ni nguzo muhimu sana katika kudumisha mahusiano kwa wanandoa. Kinyume cha hapo ni kujenga mifarakano isiyo lazoma.
7.   Kutomshukuru mwenzako anapokuwa amefanya jambo zuri; Ni vizuri inapotokea mwanaume/mwanamke kafanya jambo jema kumshukuru ili kumpa moyo wa kufanya vizuri zaidi siku nyingine. Kwa mfano kama mwanaume/mwanamke ameamua kwa upendo kukununulia zaidi ya nguo ni busara kumshukuru kwanza kwa zawadi hiyo badala ya kulaumiwa kwamba nguo hiyo siyo nzuri au imeshapitwa na wakati, umeuziwa bei mbaya, karudishe nakadhalika.
Mambo yote hayo niliyoyataja hapo juu yanaweza kuepukwa, iwapo utakuwa mtafiti  na utamweka Mungu karibu  katika maisha yako yote.  Na pia kwa ushauri naomba tuwasilianae kwa barua pepe ya fkmwamoto@gmail.com  kwa ushauri makini wa masuala ya mahusiano.



Friday, 27 June 2014

NAMNA YA KUPATA MCHUMBA

Kwa tafsiri isiyo rasmi mchumba ni mwanandoa mtarajiwa. Kabla ya kupata mchumba unapaswa kujua kanuni tatu (3) zinazohitajika katika mchakato wa kuwapata mchumba na hatimaye kuoa: -
1)   Maombi.
2)   Kutafuta.
3)   Kupata.

Naomba nifafanue kidogo kanuni hizo hapo juu:-
Maombi; Kila mwanadamu ana imani yake na kwa kupitia imani hiyo mahitaji yo yote ya muhimu kama chakula, malazi, mavazi, maisha marefu, mke mwema ni budi kumuomba yule tunayetegemea kwamba ndie mkuu na mwezeshaji wa mahitaji yetu yote (Mungu wako). Kwa hiyo, pia katika suala la kutafuta mchumba kuomba ni muhimu sana kwa maana hakuna jambo unaloweze kulipata binadamu pasipo kumuoomba Mungu wako.
Kutafuta; Baada ya kuomba kutokana na imani yako kinachofuata ni kutafuta yule mchumba uliyemuomba Mungu wako akupatie. Katika maombi yako lazima kuna wasifu unaotegemea awe nao huyo mchumba wako ambao umeomba Mungu wako akusaidie kukutafutia. Na kwa sababu Mungu wetu si mwanadamu atakupatia huyo mchumba unayemtafuta.
Kupata;
Baada ya kupata inatakiwa kuchunguza yafuatayo: -
1)   Sura yake na maumbile yake.
2)   Angalia ucha Mungu wake.
3)   Angalia tabia yake.
4)   Umri wake.
5)   Elimu yake.
6)   Fani yake.
7)   Ukoo wake.
Naomba nitoe ufafanuzi kidogo juu ya hayo mambo saba (7) yanayochunguzwa.
Sura yake na maumbile; Je, sura yake na maumbile yake yanaridhisha moyo wako? Kila binadamu hupendezwa na sura na maumbile fulani iwe mwanaume/mvulana au mwanamke/msichana. Kwa hiyo, katika hili kila mtu ana sifa anazopendelea.
Angalia ucha Mungu wake; Hapa cha kuangalia ni je, imani yake na yako ni sawa. Kama ni sawa ni vema kama si sawa je yuko tayari kujiunga na imani yako kwa roho moja na kwa dhati. Ikiwa ni hivyo ni vema, japo wengi utegeshea tu kwa lengo la kufunga ndoa na hatimaye urudia tena imani zao zamani.
Angalia tabia yake; Hapa ni kuangalia je, tabia yake inakuridhisha na inakupendeza kuwa mwenzi wako wa maisha. Kama jibu ni ndio weka vema. Kama jibu ni siyo je, anarekebishika. Kama jibu ni ndiyo jaribu kumrekebisha ukifanikiwa ni vema, chukua hatua.
Umri wake; Hapa chakuangalia ni je! umri mko sawa au amekuzidi? Kama mko sawa au amekuzidi wataalamu wa mambo ya ndoa huwa wanashauri si vizuri kwa mwanaume kuoana na mwanamke aliye mzidi kwa sababu wanawake wana kawaida ya kuzeeka haraka kwa hiyo baada ya zao kadhaa ataonekana ni mzee sana kuliko wewe. Wataalamu wa mambo ya ndoa ushauri mwanaume awe na umri mkubwa kuliko mwanamke kwa miaka kadhaa hata miaka kumi (10) ni sawa tu.
Elimu yake; Ki-elimu ni muhimu sana kuwa na tofauti ndogo sana miongoni mwao au wakawa na elimu sawa. Hii, ni muhimu sana ili kutokuwepo tofauti kubwa ya kiuelewa wa mambo mbalimbali katika jamii na urahisi wa kujichanganya katika jamii.
Fani yake; Kwa tafsiri Fani ni kazi yake inayomfanya aendeshe maisha yake kama vile uandisi, uhasibu, nesi, mwalimu, fundi cherehani; mfanyabiashara nakadhalika. Ni muhimu kujua fani yake ili kujua kama itashabihiana vipi na yako kwa mustakabali wa maisha yenu ya siku za usoni. Kama fani yake haitaleta shida upande wa malezi ya mahusiano yenu ni vema.
Ukoo/Familia wake/yake; Kwa tafsiri ya ukoo ni babu/bibi, vituku nakadhalika walikuwa na magonjwa gani ya kuridhi. Ili kwa maisha ya sasa limekuwa ni gumu sana kwa sababu ya jamii nyingi kutokuwa na mipaka katika masuala ya kuoana.
Iwapo katika vipengere hivyo saba (7) kama vitatu (3) mpaka vine (4) viko sawa ni vema ukachukua hatua ya kuoa kwa maana mambo mengine yanarekebishika mkiwa ndani ya ndoa.
Hongera kwa kuwa mwanachama wa wavuti hii, nakuomba uwaalike wenzako na ndugu zako. Nakaribisha ushauri na maoni kwa kupitia wavuti hii au kwa njia ya simu 0719841988 au 0784190882.


Monday, 23 June 2014

SIFA 14 ZA MME NA MKE BORA

MME BORA
Ahsante sana msomaji kwa kuamua kujiunga na Blogu hii awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu muumba wa mbingu na nchi kwa kunipatia uzima na ufahamu mpaka kuniwezesha kuandika machache kuhusu mada ya leo inayosomeka sifa za mwanaume bora aliyeoa.
Sifa husika ni kama zifuatazo: -
? Mcha Mungu.
? Anampenda mkewe.
? Anamheshimu mkewe.
? Mwaminifu katika ndoa.
? Ni msafi.
? Uwathamini ndugu wa mkewe sawa na ndugu zake.
? Anajua kumlinda/kumtunza mkewe na familia kwa ujumla.
? Mwenye bidii katika kazi.
? Asiwe mlevi wa kilevi aina yo yote.
? Asiwe mgomvi, mtukanaji, mtesaji, mtesi nakadhalika.
? Ni mfariji wa mkewe.
? Uomba ushauri kwa mkewe katika maamuzi muhimu ya kifamilia
? Usamehe na kuomba msamaha anapokosewa/anapokosea
? Ni huru kueleza hisia zake kwa mmewe.

Sifa hizo hapo juu pia ndio sifa bora kwa mchumba bora kwa kiume.

MKE BORA

Sifa hizo ni kama zifuatavyo:-
? Mcha Mungu.
? Anampenda mmewe.
? Anamheshimu mmewe
? Mwaminifu katika ndoa.
? Ni msafi wa mwili na anahakikisha nyumba ni safi muda wote.
? Uwathamini ndugu wa mmewe sawa na ndugu zake
? Anajua kumlinda/kumtunza/kufundisha mkewe na familia kwa ujumla.
? Mwenye bidii katika kazi.
? Asiwe mlevi wa kilevi aina yo yote.
? Asiwe mgomvi, mtukanaji, mtesaji, mtesi nakadhalika.
? Ni mfariji wa mmewe.
? Ni mshauri mkuu wa mmewe.
? Usamehe na kuomba msamaha anapokosewa/anapokosea.
? Ni huru kueleza hisia zake kwa mmewe.

Sifa hizo hapo juu pia ndio sifa bora kwa mchumba bora kwa kike.
Sifa zote za mwanaume na mwanamke zinafanana kasoro kwenye kipengere cha usafi upande wa mwanamke kuna maneno yameongezeka kidogo ya msisitizo.


Thursday, 22 May 2014

NAMNA YA KUKABILIANA NA MIGOGORO INAYOTOKANA NA WANANDOA WENYEWE

Kama nilivyoeleza kwenye makala yangu ya changamoto zinazosababishwa na wanadoa wenye mmojawapo ni mawasiliano(kutokuelewana). Hii ndio changamoto(migogoro) kubwa sana katika ndoa na ndio chanzo cha taraka nyingi kwa mujibu takwimu za kimataifa. Kwa mbaya tarakwimu za hapa kwetu nimeshindwa kuzipata kwa njia ya vyanza vyangu.
Kimsingi ni kwamba migogoro inayosababishwa na kutoelewana chanzo chake kinaweza kuwa ni mmoja wa wanadoa au wote wawili. Migogoro kikawaida ipo kwenye ndoa zote ila hutofautiana kwa kiwango. Ipo kwenye kila ndoa kutokana na sababu za malezi na tabia za asili za wanandoa. Na kawaida migogoro ukua kutokana na kukosa utayari wa kuitatua kwa wanandoa wenyewe wote wawili au mmoja wao. Inapotokea hakuna utayari kwa wote wawili ndoa haiwezi kudumu na kama ni kwa mmoja kuna asilimia fulani ndoa kuweza kudumu na kama wote wako tayari kutatua ndoa hii inakuwa na asilimia 100 kudumu.
Kama nilivyoongea kwenye makala tajwa hapo juu. Migogoro ya kutoelewana ipo inayotokana na mahitaji ya kawaida na ya kimwili. Ninavyosema mahitaji ya kawaida ni nina maana mahitaji ya msingi ya binadamu ni chakula na mavazi na mengine ambayo siyo msingi yaani; mahitaji ya kumpendezesha mwanandoa, kushaurishwa, kuthaminiwa n.k.
NAMNA YA KUPAMBANA NA MIGOGORO INAYOTOKANA NA MAHITAJI YA KAWAIDA
1.    Kuwa mkweli kuhusu hali ya kipato chako.
Kuwa mkweli wa hali yako ki-uchumi yaani; kuwa mkweli kwa mwenza wako kuhusu hali ya mapato yako. Na ukweli huu ni vizuri ufanyike kabla ya kufunga ndoa. Ni vizuri sana kama utauvaa uhalisia wako kimapato kipindi chote cha uchumba. Hili, ni muhimu sana kwa sababu ikusaidia kujua kama mchumba wako ni wa kiwango chako au la. Ukidanganya katika suala hili unakuwa umepande mgogoro ambayo itakuwa vigumu kuusuluhisha na unakuwa umejenga hali ya kutoaminika. Kwenye maelezo haya nichukulia ndoa yenye kutegemea kipato cha mwnandoa mmoja.
Pia hata pale ambapo wanandoa wote wanakipato, ni vizuri wanandoa wakawa wanajuana vipatavyo wote kwa urahisi ya kupanga mipango yao ya maendeleo kwa pamoja yenye kulingana na kipato chao.
2.    Onyesha kujali hitaji la mwenza wako.
Jitahidi kujali mahitaji ya mwenza wako kwa kumtimizia hitaji lake kama uwezo unaruhusu na kama unaona sihitaji la msingi, tafuta lugha nzuri ya kumweleza ni kwa nini unaona hitaji lisitimizwe na bila kuonyesha dalili za kupuuza au kuonyesha sihitaji la msingi.
3.    Epuka kuonyesha upendeleo katika kusaidia ndugu.
Katika familia zetu za ki-afrika kuna matatizo ya kila namna kwenye familia zetu yaani; kwa upande wa mke na mwanaume. Inapotokea kuna mahitaji upande wa familia za upande mmojawapo ni muhimu sana kuweka uwiano wa misaada inayotolea, ili kuepuka kuonyesha upendeleo.
4.    Epuka kuonyesha upendeleo kwa wageni wanao watembelea nyumbani.
Ni jambo la kawaida sana ndugu wa pande zote kutamani kuwatembelea wanandoa katika hali ya amani au matatizo. Ni vizuri kujitahidi kutoonyesha unyanyapaa kwa wanandugu wa upande mmoja hali hii inaweza kuleta mgogoro mkuu.
5.    Epuka kuonyesha dharau dhidi ya mila na desturi za mwenzi wako.
Inapotokea wanandoa ni makabila tofauti ina maana watakuwa wamekulia kataika mila na desturi tofauti. Mila na desturi uhusisha namna ya kuongea, mapishi, tofauti za ki-maendeleo baina ya kabila moja na nyingine. Si vizuri kuonyesha dharau hata kama ni katika hali ya utani kwa sababu hiyo huonyesha hisia zako dhidi ya mwenzako hata kama utasema unamtania.
6.    Epuka utani unaoeleka kweli uhalisia kimaumbile.
Jitahidi kuepuka utani unaohusiana na maumbile kama vile watu wafupi au wanene wana kasoro 1,2,3 n.k. wakati ukijua kwamba mwenza wako nao ana maumbile kama hayo. Utani kama huo hufanya mtaniwa kujisikia vibaya na kuleta migogoro katika ndoa.
7.    Kushaurishwa katika mambo ya msingi ki-familia.

Kitabia kila binadamu anapenda kuthaminiwa katika mambo tofauti tofauti kama kazi zake, ushauri n.k. Katika mambo ni pamoja na katika mambo ya msingi ya maendeleo ya kifamilia kama vile ununuzi wa kitu cho chote cha kifamilia kama vile samani, na vitu vingine muhimu katika maisha yetu ya kila siku.
 NAMNA YA KUTATUA MIGOGORO INAYOTOKANA NA MAHITAJI YA KIMWILI
Katika jamii zetu, mgogoro huu ni mkubwa sana kwa sababu takwimu zinavyoonyesha wanandoa wengi wanatoka nje ya ndoa. Takwimu hizi ni takwimu za maambulizi ya virusi vya UKIMWI. Sijafanya jitihada ya kutafuta takwimu hizi kwa sababu si jambo muhimu sana katika makala hii.

Katika hitaji hili utatuzi wake hutegemea sana mambo yafuatayo:-

ü  Uwazi wa hisia
ü  Utayari wa kujua mwili wa mwenza wako
ü  Na uwezo wake wa mwenza wako
ü  Kiwango chake cha uhitaji wake n.k.

Kifupi ni kwamba jambo hili la faragha halina kanuni maalum kwa sababu pia kuna migogoro inayotokana suala la kimaumbile, vyakula, kazi n.k.

Msingi imara wa ndoa yo yote unakuwa imara unapojengwa katika msingi ya kumtegemea Mungu kuwa kiongozi na mshauri mkuu katika ndoa.

Karibu sana UPATE MAARIFA YA KUPUNGUZA MIGOGORO KATIKA MAHUSIANO, TUJENGE TAIFA.IMARA kwa kuondoa migogoro isiyo ya lazima katika familia zetu.