Saturday, 31 March 2018

NGUVU YA KUOMBA MSAMAHA


Ingawa kuna wakati kuomba msamaha kunaonekana kama ni kitu kisichohitajika lakini ukweli ni kwamba kutokufanya hivyo kunaacha doa kubwa kuliko hata kosa ulilolifanya. Kuna nguvu katika kuomba msamaha ambayo ni kubwa kuliko maneno unayoyatamka.
Katika mafundisho yake katika mlima sermoni, Yesu alisema kuwa kama unaneno na ndugu yako na upo madhabahuni unataka kutoa sadaka, iache sadaka yako na uende kupatana naye kwanza kisha ndipo uje utoe sadaka yako.
Mathayo 5:23-24  Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako.
Hapa Yesu alimaaanisha kuwa kama umemkosea ndugu yako na hujamuomba msamaha haupaswi kufanya huduma yoyote mbele za Mungu. Haijalishi ni mtoto wako, mwenzi wako, mfanyakazi mwenzako, jirani n.k. Kuomba msamaha ni jambo gumu lakini lenye Baraka tele, kufanya hivi kutaimarisha uhusiano wako na uliyemkosea hata kama ni kwa bahati mbaya na pia kutaifanya nafsi yako kuwa huru na ya yule uliyemkosea pia.
Ni jambo baya sana kumhukumu mtu kwa jambo ambalo hajalitenda na kukataa kusikiliza upande wake wa habari na kuamini kile ulichokisikia au kuhisi. Pale unapogundua kuwa umemhukumu na kumsema mtu jambo ambalo hajafanya ni muhimu sana kumuomba msamaha kwa kutokumwamini, hii itamrejeshea heshima na upendo wake kwako na vilevile itarejeza uhusiano wenu. Inawezekana usione umuhimu wa kumuomba msamaha, lakini fahamu kuwa kutokuomba msamaha kutafanya uhusiano wenu kuwa mbaya na ni ngumu kwa mtu huyu kuachilia ulilomtendea.
Kuomba msamaha kunaondoa ile hasira aliyonayo mtu uliyemkosea na hata kama kosa ni kubwa kuomba kwako msamaha kutamfanya afikirie upya maanuzi yake na hasira yake itapungua kwa kiasi kikubwa. Ni ngumu sana kwa mtu aliyeombwa msamaha kuendelea kuwa na hasira na uchungu na Yule aliyemkosea tofauti na yule ambaye hajaombwa msamaha. Hata kama akikataa kutoa msamaha wake tatizo halitakuwa kwako tena bali kwake, moyo wako utakuwa safi na itabaki sasa yeye na moyo wake maana umeonyesha kujali kosha ulilolifanya na kulitubia.
Kumbuka, kuomba msamaha hakutakiwi kuwe ni njia ya kumlazimisha mtu uliyemkosea kukusamehe. Kama kuomba kwako msamaha kutakuwa kwa kulazimisha, kwa dharau au dhihaka au kusikomaanisha bali kwa kutimiza sheria tu kunaweza kusababisha maumivu zaidi kwa yule uliyemkosea na kuchochea hasira zaidi badala ya msamaha. Kuomba msamaha si maneno tu bali pia na vitendo vinavyofuatia na hata jinsi unavyoomba msamaha wenyewe. Maanisha kweli unachokisema na maneno yako, sauti na mwonekano mzima uonyeshe kweli umejutia kosa lako na unahitaji msamaha.
Pia usichelewe kuomba msamaha baada ya kugundua kuwa umefanya kosa. Watu wengine hawaombi msamaha hadi wasukumwe kwa maneno meengi au aone mtu amenuna na kuacha kuongea naye. Hauwezi kukaa kimya tu kama hakuna kitu kilichotokea na kutegemea kuwa jambo hilo litaisha lenyewe, unapaswa kuomba msamaha pale tu unapoona umekosea. Unapochukua muda mrefu kuomba msamaha maumivu kwa yule mtu yanazidi na hata pale unapoomba msamaha inakuwa vigumu kwake kukusamehe maana umeacha mambo yakazidi kukua ndani yake.
Ubarikiwe na Bwana Yesu unapochukua hatua na kuomba msamaha pale unapokosea. 

Kwa ushauri/maoni tunaweza kuwasiliana kwa e-mail:fkmwamoto@gmail.com au Whatsapp 0784190882.