Ingawa kuna wakati kuomba
msamaha kunaonekana kama ni kitu kisichohitajika lakini ukweli ni kwamba
kutokufanya hivyo kunaacha doa kubwa kuliko hata kosa ulilolifanya. Kuna nguvu
katika kuomba msamaha ambayo ni kubwa kuliko maneno unayoyatamka.
Katika mafundisho yake katika mlima sermoni, Yesu alisema kuwa
kama unaneno na ndugu yako na upo madhabahuni unataka kutoa sadaka, iache
sadaka yako na uende kupatana naye kwanza kisha ndipo uje utoe sadaka yako.
Mathayo 5:23-24 Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na
huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele
ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe
sadaka yako.
Hapa Yesu alimaaanisha kuwa kama umemkosea ndugu yako na
hujamuomba msamaha haupaswi kufanya huduma yoyote mbele za Mungu. Haijalishi ni
mtoto wako, mwenzi wako, mfanyakazi mwenzako, jirani n.k. Kuomba msamaha ni
jambo gumu lakini lenye Baraka tele, kufanya hivi kutaimarisha uhusiano wako na
uliyemkosea hata kama ni kwa bahati mbaya na pia kutaifanya nafsi yako kuwa
huru na ya yule uliyemkosea pia.
Ni jambo baya sana kumhukumu mtu kwa jambo ambalo hajalitenda na
kukataa kusikiliza upande wake wa habari na kuamini kile ulichokisikia au
kuhisi. Pale unapogundua kuwa umemhukumu na kumsema mtu jambo ambalo hajafanya
ni muhimu sana kumuomba msamaha kwa kutokumwamini, hii itamrejeshea heshima na
upendo wake kwako na vilevile itarejeza uhusiano wenu. Inawezekana usione
umuhimu wa kumuomba msamaha, lakini fahamu kuwa kutokuomba msamaha kutafanya
uhusiano wenu kuwa mbaya na ni ngumu kwa mtu huyu kuachilia ulilomtendea.
Kuomba msamaha kunaondoa ile hasira aliyonayo mtu uliyemkosea na
hata kama kosa ni kubwa kuomba kwako msamaha kutamfanya afikirie upya maanuzi
yake na hasira yake itapungua kwa kiasi kikubwa. Ni ngumu sana kwa mtu
aliyeombwa msamaha kuendelea kuwa na hasira na uchungu na Yule aliyemkosea
tofauti na yule ambaye hajaombwa msamaha. Hata kama akikataa kutoa msamaha wake
tatizo halitakuwa kwako tena bali kwake, moyo wako utakuwa safi na itabaki sasa
yeye na moyo wake maana umeonyesha kujali kosha ulilolifanya na kulitubia.
Kumbuka, kuomba msamaha hakutakiwi kuwe ni njia ya kumlazimisha
mtu uliyemkosea kukusamehe. Kama kuomba kwako msamaha kutakuwa kwa kulazimisha,
kwa dharau au dhihaka au kusikomaanisha bali kwa kutimiza sheria tu kunaweza
kusababisha maumivu zaidi kwa yule uliyemkosea na kuchochea hasira zaidi badala
ya msamaha. Kuomba msamaha si maneno tu bali pia na vitendo vinavyofuatia na
hata jinsi unavyoomba msamaha wenyewe. Maanisha kweli unachokisema na maneno
yako, sauti na mwonekano mzima uonyeshe kweli umejutia kosa lako na unahitaji
msamaha.
Pia usichelewe kuomba msamaha baada ya kugundua kuwa umefanya
kosa. Watu wengine hawaombi msamaha hadi wasukumwe kwa maneno meengi au aone
mtu amenuna na kuacha kuongea naye. Hauwezi kukaa kimya tu kama hakuna kitu
kilichotokea na kutegemea kuwa jambo hilo litaisha lenyewe, unapaswa kuomba
msamaha pale tu unapoona umekosea. Unapochukua muda mrefu kuomba msamaha maumivu
kwa yule mtu yanazidi na hata pale unapoomba msamaha inakuwa vigumu kwake
kukusamehe maana umeacha mambo yakazidi kukua ndani yake.
Ubarikiwe na Bwana Yesu unapochukua hatua na kuomba msamaha pale
unapokosea.
Kwa ushauri/maoni tunaweza kuwasiliana kwa e-mail:fkmwamoto@gmail.com au Whatsapp 0784190882.
Kwa ushauri/maoni tunaweza kuwasiliana kwa e-mail:fkmwamoto@gmail.com au Whatsapp 0784190882.
No comments:
Post a Comment